|
|
PROF. MAPESA ATUMIA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA KUZUNGUMZA NA WAFANYAKAZI WA MNMA
Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Haruni Mapesa amesema Chuo kinaendelea kufanya vizuri katika majukumu yake ya msingi na hii ni kutokana na Umoja, upendo na nguvu ya pamoja.
Prof. Mapesa amesema hayo leo wakati akizungumza na watumishi wa Kampasi ya Kivukoni ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma ambayo huadhimishwa kila mwaka kuanzia juni 13 hadi juni 23, ambapo hufikia kilele cha Maadhimisho hayo.
Mkuu huyo wa Chuo amewaeleza Watumishi wa Chuo hicho kuwa lengo la kuwepo kwa Wiki ya Utumishi wa Umm ...
ni kutambua mchango wa Watumishi wa Umma ikiwa ni pamoja na kukumbushana masuala ya Uwajibikaji, Maadili na Matumizi ya Mifumo ya kidijitali.
Prof. Mapesa amesema wiki hii ya Utumishi wa Umma pia inasaidia kukumbushana Wajibu na namna ya kukabiliana na Changamoto na kuzipatia ufumbuzi.
Prof. Amesisitiza kuwa Watumishi wote ni Watumishi wa Serikali hivyo suala la kufuata miongozo, nidhamu, heshima na uadilifu kwa Viongozi ni jambo la msingi pamoja na kwa mtumishi mmoja mmoja
Prof. Mapesa pia ameanisha baadhi ya Mafanikio ya Chuo kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 kuwa ni pamoja na Chuo kuendelea na ujenzi wa Jengo la Maktaba kubwa ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,500 kwa mara moja, ujenzi wa hosteli za Wanafunzi kwa Kampasi ya Karume, Ujenzi wa madarasa na ofisi za Walimu kwa Kampasi za Kivukoni.
Mafanikio mengine ni Ujenzi wa Madarasa na Ukumbi wa Mikutano kwa kampasi ya Pemba, Ujenzi wa Madarasa na Ofisi za Walimu zitakazokuwa na uwezo wa kuchukua Walimu 70 kwa Kampasi ya Kivukoni, pamoja na ujenzi wa Kantini kwa Kampasi ya Karume na Kampasi ya Pemba.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Chuo kwa ajili ya kuzungumza na Watumishi Naibu Mkuu wa Chuo anaesimamia Taaluma na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Richard Kangalawe amesema jukumu kuu la Chuo ni Kufundisha, Kufanya utafiti na kutoa Ushauri wa Kitaalamu na kuwa masuala yote yanaendelea sawa.
Naye Dkt. Evaristo Haulle anayesimamia Fedha, Utawala na Mipango amesema kuwa wiki ya Utumishi wa Umma inatoa fursa kwa Watumishi kufanya tafakuri ya Maendeleo ya Taasisi na tafakuri ya huduma tunazoItoa kwa Wadau wetu.
Katika kikao hicho pia hoja mbalimbali zilizowasilishwa na Watumishi zilipatiwa majibu, na hoja nyingine zilipokelewa kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “ Hamiza Matumizi ya Mifumo ya kidigiti ili kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano na Masoko
CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE
18.06.2025
Read more >
[ 2025-06-19 ]
|
|
|
|